Kwqa mujibu wa Shirika la Habari za Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kasuku, Kigoma, Tanzania – Darsa za maadili ya kijamii zinaendelea kutolewa katika Taasisi ya Imam Sajjad (as), iliyopo Kasuku, mkoani Kigoma, Tanzania, kupitia juhudi za watumishi wa taasisi hiyo katika kueneza mafundisho na maelekezo ya kidini yanayolenga kujenga jamii yenye misingi imara ya kimaadili na kijamii.
Miongoni mwa wanaoshiriki katika juhudi hizo ni Sheikh Rasuli Ramadhan Kwezi, ambaye ni mmoja wa watumishi wa Taasisi ya Imam Sajjad (as), anayeshiriki katika kuendeleza shughuli za kielimu na kimalezi zinazolenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu maadili na mwenendo unaopaswa kuzingatiwa katika maisha ya kila siku.

Darsa hizo zinatoa fursa muhimu ya kuwakumbusha waumini nafasi ya maadili katika maisha ya mwanadamu, hususan katika kujenga mahusiano mema baina ya watu, kuimarisha mshikamano wa kijamii, kuheshimiana, kusaidiana na kutekeleza wajibu wa kila mmoja kwa wengine.
Aidha, kuendelea kwa shughuli hizo za kielimu na kimalezi ni sehemu ya juhudi za kuhuisha mafundisho ya Ahlul-Bayt (as) katika jamii, kwa kuyafanya kuwa mwongozo wa vitendo katika maisha ya mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla.

Mafundisho ya Mtume Muhammad (saww) na Ahlul-Bayt wake watukufu (as) yanatoa msingi muhimu wa kujenga jamii inayozingatia uadilifu, huruma, uaminifu, upendo na uwajibikaji. Hivyo, darsa za aina hii zina nafasi muhimu katika kuimarisha utamaduni wa kujifunza dini na kuyatekeleza mafundisho yake katika mwenendo wa kila siku.
Kwa msingi huo, juhudi zinazoendelea kufanywa na Taasisi ya Imam Sajjad (as), Kasuku, zinastahili kuungwa mkono ili kuendeleza mwamko wa kielimu na kimaadili na kuimarisha uhusiano wa jamii na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as).

Karibuni Kasuku katika nuru ya mafundisho ya Ahlul-Bayt (as), mafundisho yanayoangaza njia ya maisha na kumwelekeza mwanadamu katika kujenga nafsi njema na jamii bora.
Maoni yako